IQNA

Muharram 1445

Ifahamu Harakati ya Mapambano ya Imam Hussein (AS)

18:40 - July 26, 2023
Habari ID: 3477343
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya mapambano ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (AS) hapo mwaka 61 Hijria dhidi ya dhulma na ufisadi wa Bani Umayya ilijaa hamasa, kujitolea na kusabilia kila kitu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo imegusa sana nyoyo za Waislamu na hata wapenda haki na kweli wasio Waislamu na kuzusha vuguvugu na hamasa ya aina yake ndani ya nafsi za wapenzi wa mtukufu huyo.

Hali hii ndiyo iliyoashiriwa na Mtume Muhammad (SAW) pale aliposema: Kuuliwa shahidi kwa Hussein kutazusha moto ndani ya nyoyo za waumini ambao kamwe hautazimika". Utabiri huo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ambao ulitolewa kabla ya mjukuu wake huyo kuuliwa shahidi umaendelea kuonekana waziwazi katika kipindi chote cha zaidi ya miaka 1400 iliyopita.

Sababu ya Harakati ya Imam Hussein (AS)

Hapa linajitokeza swali kwamba, je, harakati ya mapambano ya Imam Hussein ilichochewa na hisia kali, jazba na mihemko, au harakati hiyo ya kupigania haki na uadilifu ilifanyika kwa msingi wa akili, mantiki na kutizama mbali? Kwa kawaida akili na mantiki huarifishwa kuwa ni wenzo na chombo cha kudhamini maslahi, hali bora na raha, na aina mbalimbali za ladha na anasa za kidunia. Aina hii ya akili japokuwa ina faida wakati na mahala pake, lakini pia kuna uwezekano mkubwa kwa akili kama hii kupotoka na kuacha njia sahihi. Ni kwa kutumia akili ya aina hii ndiyo maana hii leo mwanadamu anatenda jinai za kutisha, anatengeneza silaha za maangamizi na kuyafanya mataifa mengine kuwa watumwa makoloni yake. Akili inayokusudiwa na Uislamu ni ile inayokuwa katika mipaka ya thamani aali za maadili ya kibinadamu kwa ajili ya saada na ufanisi wa mwanadamu katika maisha yake ya kidunia na huko Akhera. Mtume Muhammad (saw) anasema: Kuna aina mbili za akili, akili ya maadi (yaani ya Akhera na marejeo ya mwanadamu baada ya mauti), na akili ya maisha, kwa maana ya akili inayomdhaminia mwanadamu maisha bora na ufanisi hapa duniani. Hivyo basi akili na mantiki inayokusudiwa na Uislamu ni awamu ya juu zaidi na kamili kuliko mahesabu ya kidunia na maslahi ya kimaada na ya mtu binafsi. Akili ya Uislamu ni ile inayowadhaminia wanadamu wote, na si mtu binafsi, saada na ufanisi wa dunia na Akhera.

Mantiki ya Kiislamu

Baada ya utangulizi huo inabainika kuwa hapana shaka kwamba msingi wa harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) ulikuwa akili na mantiki ya Kiislamu iliyopata ilhamu kutoka kwenye wahyi na ufunuo na si kutokana na msukumo wa maslahi ya mtu binafsi na ya kidunia pekee. Mwanafalsafa mkubwa wa Kiirani Dakta Ghulamhussein Dinani anasema: Kimsingi Imam Hussein bin Ali (as) alikuwa picha ya akili, bali alikuwa akili iliyokuwa ikitembea baina ya watu. Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu ni akili inayotembea", mwisho wa kunukuu. 

Mwanafikra mwingine wa Iran, Hujjatul Islam Abdul Hussein Khosropanah anasema kuhusu akili na mantiki iliyotawala harakati ya Ashura ya Imam Hussein kwamba: Akili ya kidunia na kimaada inayomsukuma mwanadamu kwenye maslahi binafsi, nguvu na madaraka makubwa zaidi si akili na mantiki ya Kiashura".

Harakati ya mapambano ya Imam Hussein bin Ali (AS) iliambatana na mantiki, busara na akili tangu mwanzoni mwake. Mtukufu huyo alifuatilia kwa makini mienendo na matendo ya Muawiya bin Abi Sufiyan na kuelewa kwamba, mtawala huo dhalimu alikuwa akipotosha mafundisho ya dini na kuweka jiwe la msingi wa utawala wa mwanaye, Yazid. Harakati hiyo ya Muawiyya iliielekeza jamii ya Kiislamu katika maangamizi na upotofu mkubwa. Imam alishuhudia kwa macho kwamba, katika kipindi cha nusu karne baada ya kuaga dunia babu yake mtukufu, Muhammad (saw), watu wengi katika jamii walikuwa amekumbwa na ufisadi na mmomonyoko wa kiimani na kimaadili na hakikubakia chochote katika Uislamu isipokuwa jina lake tu. Kuchukua madaraka kwa mtu fasiki, fasidi na muovu kama Yazid bin Muawiyya kilikuwa kielelezo cha hali mbaya na maafa makubwa yaliyokuwa yameupata Umma na jamii ya Kiislamu. Katika mazingira kama hayo akili na mantiki ya Kiislamu,- na si akili ya kidunia, kimaslahi na kibinafsi,- haijuzishi wala kuruhusu kunyamaza kimya, na hutanguliza mbele suala la kuokoa dini, maadili na thamani aali kuliko maslahi ya mtu binafsi. Hii ndiyo iliyokuwa mantiki na msingi wa harakati ya mapambano ya Imam Hussein bin Ali (AS).

Mauti kwangu mimi ni saada na ufanisi

Katika kipindi chote cha harakati yake, Imam alikutana na watu waliokuwa wakifikiria maslahi yao ya kidunia pekee na mapenzi na mfungamano wao mkubwa na dunia ya kimaada viliwazuia kutambua mantiki ya mtukufu huyo na udharura wa kusimama na kupambana na dhulma, kukomboa watu na kuhuisha tena mafundisho ya Uislamu. Si hayo tu bali hata baadhi ya wapenzi wa mtukufu huyo walimnasihi kwa nia njema wakimtaka asielekea Karbala na wengine walimtaka akubali utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiyya na kuokoa nafsi yake na familia yake. Dakta Dinani anasema: "Watu ambao hawakuwa pamoja na Imam Hussein katika mpambano wa Karbala ama walikabiliana na kupigana naye au kimsingi walikuwa katika kundi potofu na batili. Wale ambao hawakuwa katika kundi hilo la batili walikuwa katika fikra za mahesabu ya maslahi ya kidunia". Kwa mujibu wa akili na mantiki ya Kiislamu, Imam Hussein (as) alikutambua kumpa mkono wa utiifu na kumkubali mtawala fasiki na muovu kama Yazid kuwa ni udhalili na fedheha kubwa ambayo ilikinzana na hadhi na nafasi yake.

Kwa msingi huo alisema waziwazi kwamba: «إِنِّیْ لا أَرَیَ الْمَوْتَ إِلَّا سَعَادَةً وَالحَیاةَ مَعَ الظّالِمِینَ إِلّا بَرَما » "Mauti kwangu mimi ni saada na ufanisi, na kuishi na madhalimu ni masaibu na tabu".  

Kuzindua Umma na kufichua maovu

Baada ya kukataa kumpa Yazid mkono wa utiifu, na kutokana na mtazamo wake wa mbali, Imam Hussein (as) aliamua kuelekea katika mji mtukufu wa Makka ambako alikaa kwa kipindi cha zaidi ya miezi minne akiwafafanulia Waislamu waliokuwa wakitokea maeneo mbalimbali ya dunia mipango ya hatakati yake na kufichua maovu ya utawala wa Bani Umayyah. Aliendelea kuzindua Umma na kufichua maovu ya utawala huo kiasi kwamba, Bani Umayya walipanga njama ya kutaka kumuua; ndipo alipoondoka katika mji huo na kuelekea Kufa nchini Iraq. Kutokana na wajibu wake wa Kiislamu, Imam aliwataka Waislamu wajiunge na harakati hiyo na marekebisho katika Umma. Baadhi ya Waislamu walijiunga na mtukufu huyo lakini wengi miongoni mwao, licha ya kukubaliana na mantiki na hoja za Imam, lakini hawakujiunga na harakati ya mapambano kwa kutumia visingizio mbalimbali vilivyotokana na mitazamo yao finyu iliyotegemea akili na mantiki ya mahesabu ya manufaa ya mtu binafsi na maslahi ya kimaada na kidunia. Imam Hussein (AS) alihubiri akili na mantiki ya Kiislamu hata katika medani ya Karbala akiwaita maadui zake katika njia ya kheri na saada ya dunia na Akhera.

Si hayo tu bali hata kuuliwa shahidi kwa mtukufu huyo na wafuasi wake waaminifu hakukuwa na sura ya kiirfani na kihamasa pekee bali walikhitari njia hiyo kwa akili timamu na maarifa kamili. Watukufu hawa walitambua vyema nafasi yao huko katika Pepo na Naima na waliamini kwamba, kumwagwa kwa damu zao kutakuwa sababu ya kuporomoka msingi wa utawala dhalimu wa Bani Umayya. Hakika Hussein bin Ali na masahaba zake wema ni kigezo na ruwaza njema kwa wapigania uhuru na haki si katika zama zao pekee bali zama na nyakati zote.

Mapambano ya Ashura

Katika upande mwingine kukamatwa mateka watu wa familia ya Mtume (SAW) katika mapambano ya Ashura kuligeuka na kuwa sababu ya kutangaza malengo ya harakati ya Imam Hussein na kufichua uovu na uozo wa utawala wa Yazid na Bani Umayya.

Wanafikra na wasomi wamekuwa wakitafuta jibu la swali kwamba, je, akili na mantiki ya harakati ya mapambano ya siku ya Ashura inaoana na penzi, vuguvugu na hamasa yake? Baadhi ya watu wanadhani kuwa, harakati hiyo ya Imam Hussein ilisimama katika msingi wa hisia kali, jazba na mihemuko bila ya kutilia maana akili na mantiki. Hii ni kwa sababu,- wanasema watu hao,- akili na mantiki havimuamuru mtu kufanya harakati ambayo hatima yake ni kuuliwa shahidi. Katika upande mwingine wanazuoni wa Kiislamu wanaamini kwamba, katika dini ya Uislamu hakuna mtengano baina ya akili na kuashiki na kwamba mantiki na akili katika awamu yake ya juu kabisa hufikia daraja ya kuyeyuka na kuifia katika dhati ya Mwenyezi Mungu SW. Ustadh Ghulam-Hussein Dinani anasema: Upatanifu, mwafaka na muoano wa akili na penzi ambao ndiyo njia ya moja kwa moja ya kufika kwa Mwenyezi Mungu SW hujulikana kwa jina la "tariqa". Tariqa ndiyo njia isiyo na wasita ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na katika njia hiyo hakuna mtengano baina ya akili na penzi. Akili na kuashiki ni pande mbili za sarafu moja".

Ustadh Dinani anamalizia kwa kusema: Imam Hussein (AS) alikuwa akili iliyokuwa ikitembea lakini akili iliyodhihiri katika sura ya kuashiki na kuipenda dhati ya Mwenyezi Mungu mtukufu. Hilo lilikuwa penzi la akili. Akili ya Imam Hussein ilikuwa penzi na kumuashiki Allah SW, na penzi lake hilo lilikuwa akili na mantiki yake.

Kwa utaratibu huo, mpenzi msikilizaji, japokuwa masuala kama kusabilia nafsi, kujitoa mhanga, kufa shahidi, kulinda izza na kupambana na dhulma hakuna maana katika kamusi ya akili ya kimaada ambayo inayatambua masuala hayo kuwa yanachochewa na hisia kali, mihemuko na jazba zisizo na mantiki, lakini mambo hayo katika akili na mantiki ya Uislamu inayojali ufanisi wa dunia na Akhera ni sahihi na yenye misingi madhubuti. Akili na kuashiki au kupenda katika mwanga wa wahyi na ufunuo ni mithili ya mbawa mbili za ukamilifu wa mwanadamu, na huu ndio uhakika uliodhihiri kikamilifu katika tukio la siku ya Ashura. 

Habari zinazohusiana
Kishikizo: ashura imam hussein as
captcha