IQNA

Hamas yalaani Uingereza kwa kuiweka katika orodha ya 'makundi ya kigaidi'

16:57 - November 19, 2021
Habari ID: 3474577
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa taarifa ya kulaani uamuzi uliojaa chuki wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza wa kuiweka harakati hiyo katika orodha ya 'makundi ya kigaidi.'

Katika taarifa hiyo, Hamas imesema: "Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Priti Patel, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza ametangaza kuwa eti Hamas ni kundi la kigaidi na wanaoiunga mkono harakati hii wametishiwa na kifungo cha miaka 10 gerezani."

Hamas imeongeza kuwa,  "inasikitisha kuona kuwa Uingereza inaendeleza ujinga wake wa huko nyuma ambapo badala ya kuliomba radhi taifa la Palestina na kurekebisha makosa yake ya kihistoria iwe ni katika kutoa ahadhi chungu wakati wa azimio la Balfour au ukoloni wake Palestina na kisha kisha kuikabidhi ardhi hii kwa Wazayuni, sasa inaunga mkono uvamizi wa maghasibu dhidi ya taifa linalodhulumiwa la Palestina."

Ikumbukwe kuwa Azimio la Balfour ndilo ambalo lilipelekea kuundwa utawala bandia wa Israel ambao sasa unazikoloni na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina ukiwemo mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) uliko Msikiti wa Al Aqsa ambao ni qibla cha kwanza cha Waislamu.

Hamas imesisitiza kuwa, mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutumia mbinu zote zinazowezekana zikiwemo silaha ni kwa mujibu wa sheria za kimataifa na ni haki ya kimsingi ya taifa lolote ambalo ardhi zake zinakaliwa kwa mabavu. Aidha taarifa hiyo imesema utawala wa Kizayuni wa Israel mbali na kuwa unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina pia unawaua kwa umati  na kubomoa nyumba zao na kwa muda wa miaka 15 sasa umelizingira eneo la Ukanda wa Ghaza na kuwaathiri vibaya wakazi milioni mbili wa eneo hilo ambao aghalabu ni watoto. Katika kuuzingira Ukanda wa Ghaza Israel imetekeleza jinai dhidi ya binadamu na hilo limethibitishwa na taasisi huru za kutetea haki za binadamu katika uga wa kimataifa.

Hamas imeitaka Uingereza isitishe mara moja uungaji mkono kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na imetoa wito kwa watu huru duniani na waungaji mkono wa Palestina walaani vikali uamuzi huo wa Uingereza.

Aidha Hamas imesisitiza kuwa watu wa Palestina, umma wa Kiislamu, mataifa ya Kiarabu na wapenda uhuru kote duniani wataendeleza harakati zao za kupigania uhuru na wapinzani hawawezi kuwazuia katika njia hii.

Baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza kutangaza Ijumaa kuwa eti Hamas ni kundi la kigaidi, kama ilivyotarajiwa, utawala dhalimu wa Israel, ambao utambulisho wake halisi ni wa kigaidi, umeunga mkono uamuzi huo.

4014489

captcha