IQNA

Harakati ya Qur'ani

Iran yafungua Kituo cha Kitaifa cha Tarjama ya Qur'ani Tukufu

11:39 - January 30, 2024
Habari ID: 3478275
IQNA - Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuzindua kituo cha tarjama au tarjuma ya Qur'ani Tukufu.

Hayo ni kwa mujibu wa Ali Reza Moaf, Naibu Waziri na Mkuu wa Masuala ya Qur'ani na Etrat wa Wizara ya Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu ya Iran. Aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Tehran.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, maafisa wa wizara hiyo walibainisha mafanikio na mipango 14 ya Qur'ani Tukufu katika wizara hiyo..

Moja ya mipango hiyo ni "kuanzishwa kwa Kituo cha Kitaifa cha Tarjama ya Qur'ani cha Jamhuri ya Kiislamu," Moaf alisema, akibainisha shughuli za kituo hicho zilianza tangu Jumatatu.

Kituo hicho kitakuwa na baraza la tarjama litakalojumuisha wataalamu wa ngazi za juu wa Qur'ani Tukufu nchini, aliongeza.

Mpango mwingine ulioanzishwa katika hafla hiyo ulikuwa "Mkataba wa Qur'ani Tukufu wa Mfumo wa Utawala a Sekta za Utamaduni na Sanaa."

"Waraka huu unaonyesha maelezo mahususi ya jinsi sinema, ukumbi wa tamthilia, na sanaa zingine zinaweza kuendana na kanuni za Qur'ani Tukufu" afisa huyo alisema.

Mpango mwingine ulioanzishwa unalenga kuwahimiza wanaharakati wa Qur'ani kuwa watendaji zaidi kwenye mitandao ya kijamii, kuitangaza Qur'ani miongoni mwa watumiaji wa majukwaa mbalimbali ya kijamii.

Kuzindua kozi ya elimu ya Qur'ani kwa umma na kuanzisha jumuiya za kimataifa za Nahj al-Balagha na Sahifa al-Sajjadiyya ilikuwa miongoni mwa mipango mingine iliyotangazwa.

4196742

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu iran
captcha