IQNA

Mahakama ya Umoja wa Mataifa kuanza tena kusikiliza kesi ya mauaji ya Waislamu wa Rohingya

14:54 - February 21, 2022
Habari ID: 3474954
TEHRAN (IQNA)- Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) leo Jumatatu inaanza kusikiliza tena kesi ya mauaji ya Waislamu wa Rohingya wa Myanmar iliyokuwa imewasilishwa na Gambia katika mahakama hiyo.

Kesi hiyo inaanza kuusikilizwa leo huku kukiwa na mjadala endapo watawala wa sasa wa kijeshi nchini Myanmar watahudhuria kesi hiyo au la.

Duru za karibu na mahakama hiyo zinasema kuwa, kesi hiyo iliyowasilishwa na Gambia kwa niaba ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inatarajiwa kuendeshwa kwa muda wa siku nne.

Katika mashtaka yake hayo, Gambia inaituhumu serikali ya Myanmar kwamba, imefanya mauaji kupitia jeshi lake dhidi ya jamii ya walio wachache ya Waislamu wanaoishi katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo.

Serikali ya Gambia imekuwa ikisisitiza kuwa, imechukua hatua hiyo ili kutafuta haki na kuhakikisha kuwa, wahusika wa mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Myanmar dhidi ya Warohingya wanabebeshwa dhima.

Gambia iliwasilisha faili la kesi ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Warohingya katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) mwaka 2019.

Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuliwa, laki nane wamejeruhiwa na wengine wapatao milioni moja wamelazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh ili kunusuru maisha yao, baada ya jeshi na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka kuanzisha mauaji ya kinyama Agosti 25 mwaka 2017.

3477891

captcha