IQNA

Ufaransa yaanza mpango wa kufunga msikiti karibu na Paris

19:43 - December 15, 2021
Habari ID: 3474678
TEHRAN (IQNA)-Ufaransa imeendeleza sera zake dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kuanzisha mpango wa kufunga msikiti mmoja katika mji wa Beauvais kwa muda wa miezi sita kutokana na kile kilichodaiwa ni hotuba zenye misimamo mikali msikitini hapo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin amedai kuwa hotuba katika msikiti huo ‘hazikubaliki’ kwa sababu Imamu amekuwa akizungumza kuhusu Wakristo na Mayahudi.

Mji wa Beauvais uko umbali wa kilomita 100 kutoka mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

Wakuu wa mji huo wanasema wanatafakari kutoa adhabu ya kuufunga msikiti huo kwa muda wa miezi sita kutokana na kile ambacho kimedai ni hotuba zinazochochea chuki na ghasia.

Samim Blaki, wakiri wa kamati ya msiki huo amesema tuhuma hizo zinahusu matamshi ya Imamu wa kujitolea ambaye alizungumza kinyume cha taratibu lakini alikatazwa kufanya hivo.

Hatahivyo wakuu wa mji huo wanasema mhubiri huyo hutoa hotuba mara kwa mara katika msikiti huo na kwamba hushambulia itikadi za jamii za kimagharibi.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa inasema misikiti na kumbi za sala 99 kati ya 2,623 kote katika nchi hiyo zimechunguzwa miezi ya hivi karibuni  

Tayari misikiti 21 imefungwa na sita inachunguzwa na yamkini ikafungwa kwa mujibu wa sheria za Ufaransa.

Kwa muda sasa kumekuwa kukishuhudiwa wimbi jipya la vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu ambapo misikiti imekuwa ikilengwa. 

Ufaransa ina idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016, kuna zaidi ya Waislamu milioni 5.7 Ufaransa ambao ni takribani asilimia 8.8 ya watu wote nchini humo.

4020969

captcha