IQNA

Rais Hassan Rouhani

Iran inasisitiza kuimaarishwa uhusiano wa nchi za Kiislamu

7:04 - April 15, 2016
Habari ID: 3470247
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kuimarishwa uhusiano baina ya nchi za Kiislamu ni kati ya vipaumbele vya awali vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rais Hassan Rouhani amesema Alhamisi katika Kikao cha 13 cha Viongozi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Istanbul Uturuki kuwa, hii leo ambapo wanachama wa jumuiya hiyo wamekutana katika mji wa Istanbul kwa nara za " Umoja na Mshikamano kwa ajili ya Uadilifu na Amani", ni fursa nzuri kwa ajili ya kufikiria mustakbali wa pamoja wa Waislamu ulimwenguni kote.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, harakati yoyote yenye lengo la kuzusha mgawanyiko ndani ya Jumuiya ya OIC haina itibari wala nafasi na kwamba, hitilafu zinazoukabili Ulimwengu wa Kiislamu ni suala la pamoja. Amesema kupatiwa ufumbuzi hitilafu hizo na suutafahamu nyingine, kunawezekana tu kupitia udiplomasia na kwa kustafidi na njia nyingine za amani na kufanyika mazungumzo.

Rais Rouhani ameashiria kuongezeka makundi yenye misimamo ya kufurutu ada, hitilafu na mizozo ya kimadhehebu katika Ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa, kuporomoka utamaduni wa Kiislamu kulianza wakati madola makubwa ya Kiislamu yalipoanza kuzozana yenyewe kwa yenyewe bila ya manufaa yoyote badala ya kushikamana pamoja; na hivyo kutayarisha mazingira ya uvamizi kutoka nje.

Rais wa Iran amesema anasikitishwa na misaada ya kifedha na kijeshi inayotolewa na baadhi ya nchi kwa makundi yaliyo dhidi ya Uislamu kwa lengo la kuzinasibisha jinai na mauaji na dini Tukufu ya Uislamu na kueleza kuwa, nchi za Kiislamu zilizopo kwenye Muungano wa Kimataifa kwa ajili ya Amani na Kupambana na vitendo vya Ukatili, kwa jina la Uislamu zinapasa kusaidia kurejesha amani ya kudumu na haki za pande zote za wanadamu katika eneo na ulimwenguni kwa ujumla.

Rais Rouhani ameutaja utawala wa Kizayuni kuwa ni chanzo kikuu cha vitendo vya ukatili na uchupaji mipaka na kueleza kuwa, kuendelea kuuliwa kwa umati raia wa Palestina na kuzingirwa Ukanda wa Ghaza, kunaashiria wazi asili ya utawala unaopenda mabavu ambao unapata kiburi cha kuendeleza ukatili na ukandamizaji wake kutokana na kimya na upuuzaji wa jamii ya kimataifa khususan madola ya Magharibi.

Rais Rouhani amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa na inaendelea kuziunga mkono na kuzitetea nchi za Kiislamu na Waislamu mbele ya uvamizi, vitisho, ukaliaji mabavu na ugaidi.

3488639

captcha