IQNA

Bahrain yavunja misikiti na kujenga kanisa kubwa

17:11 - July 05, 2014
Habari ID: 1426057
Katika hali ambayo utawala wa kifalme wa Bahrain hadi sasa umeshavunja misikiti 38 nchini humo kwa visingizio tofauti, Mfalme wa Bahrain amemzawadia Papa Francis wa Kanisa Katoliki, ramani ya kanisa kubwa linalotarajiwa kujengwa nchini humo.

Taarifa zinasema kuwa, Hamad bin Isa Aal Khalifa, Mfalme wa ukoo wa Aal Khalifa wa Bahrain  aliitembelea Vatican na kukutana na Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duaniani na kujadiliana naye masuala mbalimbali kama vile amani katika Mashariki ya Kati, kuishi pamoja kwa usalama na amani wafuasi wa dini tofauti na kukabiliana na makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka katika dini. Aidha Utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain umetoa msaada wa kitita cha dola milioni 30 kwa ajili ya kujengwa kanisa hilo kubwa zaidi la Kikatoliki katika Mashariki ya Kati.Kanisa hilo linalotarajiwa kujengwa nchini Bahrain litakuwa kubwa zaidi kuwahi kujengwa katika nchi za Kiarabu. Wapinzani wa Bahrain wanasema kuwa, safari ya Mfalme wa Baharin huko Vatican ni hatua ya kimaonesho yenye lengo la kusafisha taswira ya utawala huo wa kidhulma ambao kwa miaka kadhaa unawakandamiza raia wanaoandamana kwa amani, hasa Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo. Tangu kuanza harakati za mapinduzi za wananchi wa Bahrain mwaka 2012 hadi sasa, zaidi ya watu 150 wameshapoteza maisha yao kutokana na ukandamizaji unaofanywa na utawala wa ukoo wa kifalme wa Bahrain huku mamia wakitiwa mbaroni kwa sababu tu ya kuandamana na kudai haki zao za kimsingi.

Utawala wa Aal Khalifa unajaribu kuibadili nchi hiyo na kuwa kituo kikuu cha maaskofu wa kanisa Katoliki sambamba na kumhamishia huko Manama mji mkuu wa Bahrain Askofu Camillo Ballin Mkuu wa Wakatoliki nchini humo, katika hali ambayo Wakatoliki nchini humo ni chini ya watu laki moja, wengi wao wakiwa ni wafanyakazi wahamiaji kutoka Ufilipino, India na Sri Lanka .

1425682

 

captcha