IQNA

OIC yalaani ugaidi wa Boko Haram nchini Nigeria

22:04 - February 28, 2014
Habari ID: 1380935
Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC imetoa taarifa na kulaani hujuma ya hivi karibuni ya kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi ya shule moja nchini Nigeria ambapo wanafunzi 57 waliuawa.

Kwa mujibu  wa mwandishi wa  Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, Katibu Mkuu wa OIC Iyyad Madani ametoa taarifa na kulaani vikali hujuma ya siku ya Jumatatu ya magaidi wa Boko Haram dhidi ya shule moja katika jimbo la Yobe. Ametoa wito kwa serikali ya Nigeria kuhakikisha waliotenda jinai hiyo wanafikishwa kizimbani. Madani amesema OIC inalaani vikali ugaidi na misimamo mikali ambayo amesema inakiuka mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
Kwingineko, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani hujuma ya kigaidi ya kundi la Boko Haram dhidi ya shule katika  jimbo hilo la Yobe nchini Nigeria. Bi. Marzieh Afkham amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia misingi yake ya siku zote, inalaani utumiaji nguvu, misimamo mikali na vitendo vya kigaidi hasa kitendo kilicho dhidi ya binadamu cha hivi karibuni katika Jimbo la Yobe Nigeria. Amesema Iran inalitakia taifa la Nigeria utulivu na usalama.
Wakati huo huo, Ijumaa hii serikali ya Nigeria imetangaza vita kamili dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limekuwa likifanya mauaji nchini humo.
Doyin Okupe msemaji wa Ofisi ya Rais wa Nigeria amesema mgogoro ulioibuliwa na Boko Haram ni vita kamili. Amesema serikali ya Nigeria inakabiliana na adui mkubwa sana ambaye sasa amechukua mwelekeo wa kimataifa.  Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Maelfu ya watu wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009. Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.
1380850

Kishikizo: BOKO HARAM nigeria oic
captcha