IQNA

Salamu za Idul Fitr

Rais wa Iran: Ni wajibu kwa nchi za Kiislamu kukomesha jinai za Israel huko Gaza

10:34 - April 10, 2024
Habari ID: 3478661
IQNA-Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, amesema ni wajibu wa kibinadamu na kidini kwa nchi za Kiislamu kukomesha mauaji ya kimbari ya miezi kadhaa ya utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Sayyid Ebrahim Raisi ametoa kauli hiyo katika ujumbe wake kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Fitr, ambayo inaadhimishwa kuanzia leo baada ya kumalizika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

"Nchi za Kiislamu zina wajibu wa kibinadamu na wa kidini wa kusimamisha haraka mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Iisrael, ambayo ni jinai dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari, na kupunguza mateso ya watu wasio na ulinzi wa Gaza," amesema Rais wa Iran.

Raisi amesema Iran iko tayari kwa ushirikiano wowote ndani ya fremu ya mipango ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutatua tatizo la njaa na majanga mengine ya kibinadamu huko Gaza.

Akipongeza maandamano ya kimataifa ya kuwatetea Wapalestina katika Siku ya Kimataifa ya Quds, iliyoadhimishwa katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, Sayyid Raisi amesema: "Ni lazima kutumia mahudhurio haya yenye thamani kubwa kukomesha mashambulizi na mzingiro wa Gaza unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel na kutuma misaada ya kibinadamu."

Israel ilianzisha mashambulizi ya kikatili kwenye Ukanda wa Gaza, yakilenga hospitali, makazi ya raia na nyumba za ibada, baada ya harakati za Muqawama wa Palestina kufanya Operesheni ya Kimbunga ya al-Aqsa dhidi ya utawala huo ghasibu tarehe 7 Oktoba.

Hadi sasa utawala huo haramu umeuwa zaidi ya Wapalestina 33,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Israel pia imezuia maji, chakula na kukata umeme kwa eneo la Gaza, na kulitumbukiza katika mgogoro mkubwa wa binadamu.

 

4209764

captcha