IQNA

Kiongozi Muadhamu: Waliomuua mwanachuoni wa Kisunni wanataka kuwagawanya Wairani

20:55 - December 14, 2022
Habari ID: 3476248
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelaani kitendo cha kutekwa nyara na kuuawa mwanachuoni wa Kisunni huko kusini mashariki mwa Iran na kusisitiza kuwa, watenda jinai waliotekeleza uhaini huo wanatumikia maslahi ya pande zinazopinga ustawi na umoja wa wananchi wa Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo katika ujumbe wake uliotolewa leo Jumatano, ambapo ameeleza kusikitishwa na tukio hilo chungu, huku akitoa mwito kwa mamlaka husika kuwakamata na kuwafikisiha mbele ya sheria wahusika wa jinai hiyo.

Ayatullah Khamenei amesema katika ujumbe huo kuwa: Tukio chungu la kutekwa na kuuawa shahidi Mowlavi Abdolvahed Rigi, Imam wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Khash katika mkoa wa Sistan na Baluchestan limeibua simanzi na masikitiko makubwa.

Kiongozi Muadhamu amemtaja marehemu Rigi kama mwanachuoni mahiri na shujaa, huku akivitaka vyombo vya dola kufanya hima ili watekelezaji wa mauaji ya msomi huyo wabebeshwa dhima ya jinai yao.

Aidha ametoa mkono wa pole kwa familia, jamaa na vilevile wakazi wa mkoa wa Sistan na Baluchestan hususan wa miji ya Khash na Iranshahr, kwa kuondokewa na msomi huyo mashuhuri wa Kisunni.

Sehemu moja ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu inasema: Wahalifu waliotenda jinai hiyo ni mamluki wa maadui wanaopinga maendeleo ya Wabaluchi na umoja wa taifa zima la Iran.

Mwili wa mwanachuoni huyo ulipatikana Ijumaa iliyopita pembeni ya barabara katika mji wa Kash katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, kusini mashariki mwa Iran, siku moja baada ya kutekwa nyara kutoka msikitini na watu wasiojulikana.

Wizara ya Intelijensia ya Iran jana Jumanne ilitoa taarifa ikisema kuwa, magaidi watatu wanaoshukiwa kuhusika na utekaji na mauaji ya msomi huyo wa Kiislamu wametiwa nguvuni, wakijaribu kutoroka nchini.

3481669

captcha