IQNA

Vita vya Saudia dhidi ya Yemen

Mkuu wa Ansarullah aushauri Muungano wa Saudi Arabia usitishe vita Yemen

16:08 - August 24, 2022
Habari ID: 3475675
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi wa harakati ya muqawama (mapambano) ya Ansarullah ya Yemen ameushauri muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia kuchukua fursa ya usitishaji vita ili kukomesha uvamizi wake dhidi ya Yemen sambamba na kusitisha mzingiro wake dhidi ya nchi hiyo.

Wakati wa hotuba ya televisheni siku ya Jumanne, Abdul Malik al-Houthi alisema kuwa haikuwa rahisi kwa Yemen kupata mbadala wa mapato wakati muungano wa Saudia ukiwa umdumisha mzingiro.

Aidha amesema mtu yeyote, ambaye hatalitazazama kwa uzito na kipaumbele suala la kukabiliana na wavamizi , "anapuuza ukubwa na malengo ya uvamizi huu," Al Houthi aliongeza, akiwataka Wayemen kushikilia misimamo yao kuhusu uhuru wa nchi.

Aliendelea kusema kuwa licha ya kusitishwa mapigano kwa muda, vikosi vya Yemen vinahifadhi utayari wao kamili wa kukabiliana na malengo maovu ambayo huenda yanafuatiliwa na wavamizi wa nchi hiyo.

"Moja ya vipaumbele vyetu wakati wa kipindi cha usitishaji mapigano kwa muda ni kuhifadhi kiwango cha juu cha utayari na kuzingatia njama zote za maadui," Houthi alisema.

"Licha ya kudumisha utayari wetu katika kipindi cha sasa cha kusitisha mapigano, hatupaswi kudhani kuwa vita vimekwisha na kuanza kujihusisha na masuala mengine," aliongeza.

Kwingineko katika hotuba yake, Abdul Malik al-Houthi alisema rasilimali zote za mafuta na gesi za Yemen zimeporwa na "muungano wavamizi, wezi, na maghasibu."

Saudi Arabia ilianzisha vita vikali dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa ushirikiano na washirika wake wa Kiarabu na kwa msaada wa silaha, vifaa na kisiasa kutoka Marekani na mataifa mengine ya Magharibi.

Lengo lilikuwa kuuweka tena utawala rafiki wa Riyadh wa rais wa zamani wa Yemen, Abd Rabbuh Mansur Hadi, na kukandamiza vuguvugu la Ansarullah, ambalo limekuwa likiendesha masuala ya serikali.

Makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yalianza kutekelezwa mwezi Aprili kati ya muungano huo na Ansarullah. Makubaliano hayo yameongezwa mara mbili tangu wakati huo.

Vita vilivyoanzishwa  na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen na kuendelea hadi sasa vimeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha mamilioni wakiwa hawana pa kuishi. Aidha vita hivyo vimesababisha matatizo mengi ya ukosefu wa chakula, matibabu na elimu kwa watu wa Yemen.

Katika kulipiza kisasi jinai hizo, Jeshi la Yemen hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maeneo ya kistratijia ya Saudi Arabia na UAE.

3480203

 

captcha