IQNA

Njama za Wazayuni

Mwanazuoni wa Lebanon alaani Saudia kutumia Hija kuanzisha uhusiano na Israel

18:14 - July 12, 2022
Habari ID: 3475494
TEHRAN (IQNA) – Mwanazuoni wa Lebanon na katibu mkuu wa Umoja wa Wanazuoni wa Muqawama au Mapambano ya Kiislamu amelaani vikali ufalme wa Saudia kwa kumteua mhubiri anayeunga mkono utawala haramu wa Israel kuongoza Sala wakati wa Siku ya Arafah wakati wa Hija.

Sheikh Maher Hamoud alisema Saudi Arabia imetumia Hija ya kila mwaka kama lango la kurejesha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni  wa Israel.

Alisema mamlaka ya Saudia ilimteua Sheikh Mohammad al-Issa kuwa kiongozi wa sala na mhubiri wa Msikiti wa Namira katika Siku ya Arafah, ambayo ni kati ya nguzo za Hija.

Hii ni wakati al-Issa, ambaye pia ameteuliwa kama katibu mkuu wa Jumuiya ya Ulimwengu ya Waislamu, amefanya vitendo visivyo vya kimaadili ambavyo vinaenda kinyume na kanuni za kimsingi za Uislamu, Sheikh Hamoud alisema.

Ameongeza kuwa al-Issa ni mtu ambaye amewaita Wazayuni ndugu zake na kuwataja wapiganaji wa Kipalestina na watetezi wa Msikiti wa Al-Aqsa kuwa ni magaidi.

Sheikh Hamoud alisikitishwa na ukimya wa mamlaka ya Saudia juu ya hasira ya wanazuoni wa Kiislamu katika uteuzi wa al-Issa.

Al-Issa mwaka 2020 alitembelea kambi ya zamani ya mateso ya Wanazi ya Auschwitz nchini Poland pamoja na kundi la Wayahudi, siku chache kabla ya utawala wa Tel Aviv kwenda kuadhimisha mauaji ya Holocaust katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa Kizayuni

Saudi Arabia iko katika mkakati wa kuweka wazi uhusiano wake wa siri wa miaka mingi na utawala wa Israel. Inatazamiwa kuwa uhusiano wa Tel Aviv na Riyadh utachukua sura mpya wakati wa safari ya Rais Joe Biden nchini Saudia wiki hii.

4070262  

captcha