Akizungumza na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA) Ijumaa, Hujjatul-Islam Mohammad Hassan Aboutrabi Fard alipongeza utendaji wa Waislamu katika ibada ya Hija hasa kwa kuzingatia washiriki ni kutoka kaumu mbali mbali.
"Moja ya nembo muhimu za Hija ni kujenga jamii ambayo wanadamu kutoka kaumu na mataifa tofauti kutoka ulimwenguni kote hukusanyika mahali salama kwa mujibu wa maadili yatokanayo na mafundisho ya kidini na kibinadamu na hufanya ibada yenye muelekeo wa kidini, kisiasa na kijamii kwa utaratibu na nidhamu kamili," amesema.
Ameitaja Hija kuwa ni fursa ya kukuza Uislamu zaidi, na kuongeza wamba jukumu la wasomi na viongozi wa Kiislamu ni kuelezea kuhusu misingi ya hali ya juu ya Hija kwa ulimwengu na kwa kufanya hivyo, kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na Kizayuni ambavyo vina bajeti maalumu ya kuwasilisha taswira potovu na isiyo sahihi ya Uislamu.
Hija ni moja wapo ya nguzo za Uislamu kwamba Waislamu ambao wana uwezo wanapaswa kutekeleza ibada hii angalau mara moja katika maisha yao. Waislamu kawaida huweka akiba kwa miaka kadhaa ili kushiriki katika ibada hiyo.
Hija inajumuisha ibada ambayo huchukua zaidi ya siku tano katika mji mtakatifu zaidi wa Kiislamu Makka, na maeneo ya karibu ya Saudi Arabia ya Magharibi.