IQNA

Spika wa Bunge la Iran

Nchi za Magharibi zimewadhalilisha wazee katika janga la corona

21:41 - May 03, 2020
Habari ID: 3472729
THERAN (IQNA) - Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu, Bunge la Iran, amesema katika kadhia ya ugonjwa wa corona (COVID-19), ubinadamu umeporomoka na kadhia hii inatazamwa kibiashara.

Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran, ambaye hivi karibuni alipona baada ya kuugua corona, amehutubu katika kikao cha bunge Jumapili na kusema katika kukabiliana na corona, Wamagharibi wamewaambia wazee katika jamii zao kuwa hawatakiwi tena kwa sababu hawana faida kwa uchumi.

Larijani ameashiria hatua za Iran katika kukabiliana na corona na kusema wananchi wa Iran, wakiwemo wafanyakazi wa sekta ya tiba, wana moyo wa kujitolea na wa kijihadi ambapo wameamiliana kwa heshima na watu wote, hasa wazee, katika kuwapa matibabu.

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema, kutokana na jitihada hizo, takribani asilimia 80 ya wote walioambukizwa corona nchini Iran wameweza kupata nafuu na kuruhusiwa kuenda nyumbani baada ya matibabu.

Larijani aidha ameashiria Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi iliyoadhimishwa Mei Mosi na kusema: "Wafanyakazi Wairani  wamejitolea muhanga katika kupambana na Marekani ambayo imiliwekea taifa la Iran vikwazo." Amesema wafanyakazi wa Iran hawataruhusu ndoto za watawala wa Marekani kuhusu Iran zitimie.

3895998

captcha