IQNA

Waislamu wanaoteswa Myanmar wamesahaulika

9:34 - March 17, 2016
Habari ID: 3470202
Maelfu ya ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa na makumu maelfu ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Umoja wa Mataifa pia umetangaza kuwa Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar ni moja kati ya jamii zinazodhulumiwa zaidi duniani.

Massoud Shhadjareh, mkuu wa Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu yenye makao yake London anasema Waislamu nchini Maynmar wanabaguliwa na jeshi la nchi hiyo pamoja na vyama vya kisiasa vinavyodai kuwa vya kidemokrasia.

Katika mahojiano na Press TV amezungumza kuhusu uamuzi wa bunge la Myanmar kumchagua Htin Kyaw kuwa rais mpya wa nchi hiyo. Kyaw ni mpambe na mashirika wa karibu wa Aung San Suu Kyi kiongozi wa upinzani ambaye anazuiwa na sheria kuwa rais kutokana na kuwa na uraia wa nchi mbili. Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo.

Swali: Je tunashuhudia mwanzo mpya katika siasa za Myanmar?

Jibu: Ukweli ni kuwa, tunashuhudia kumalizika utawala wa kijeshi lakini sioni mabadiliko yoyote kuhusu Waislamu wa Myanmar.

Swali: Unaweza kufafanua zaidi kuhusu kadhia ya Waislamu wa kaumu ya Rohingya?

Jibu: Nukta ya pamoja ya Jeshi na vyama vya kidemokrasia Myanmar ni kuwa pande mbili zinapinga kuwatambua Waislamu Myanmar kama raia wenye haki. Hata Aung San Suu Kyi binafsi alipoulizwa kuhusu Waislamu wa Myanmar alisema anaamini kuwa si sehemu ya jamii ya nchi hiyo na kwamba ni raia wa kigeni. Kwa hivyo nadhani kuna ushirikiano baina ya jeshi na harakati za kidemokrasia na hapa Waislamu dnio wahanga. Ukweli ni kuwa Waislamu Myanmar wanapaswa kupewa haki ya uraia lakini hatua hatua yoyote ikichukuliwa kuwapa haki zao na kuwalinda.

Swali: Je unadhani kwa kuchaguliwa serikali ya kwanza ya kiraia Myanmar baada ya miongo kadhaa kunaweza kushuhudiwa kuboreka hali ya Waislamu wa Rohingya.

Jibu: Ni jambo la kusikitisha kuwa, kwa kuzingatia matamshi ya huko nyuma, hakuna matumaini sana. Sisi kama jumuia za kiraia kimataifa tutakuwa na watu wa Myanmar katika kuishinikiza serikali mpya itende haki na uadilifu. Tunataka kuwepo suluhisho linalokubalika kimataifa kwa ajili ya kuwapa Waislamu wa Myanmar haki na uadilifu kwani wamekuwa wakidhulumiwa kwa muda mrefu. Iwapo serikali ya sasa inataka uhalali, basi inapaswa kusuluhisha kadhia ya Waislamu wa Myanmar.

3459349

captcha