IQNA

Mabudhha wadai ushindi Myanmar, Waislamu wazidi kutengwa

12:54 - September 07, 2015
Habari ID: 3360047
Mabudhha wenye misimamo mikali nchini Myanmar tayari wametangaza 'ushindi' dhidi ya Waislamu nchini humo katika uchaguzi utakaofanyika Novemba baada ya kupitishwa sheria tata dhidi ya Waislamu ambayo inawanyima Waislamu wa kabila la Rohingya haki ya kupiga kura.

Kiongozi mwenye misimamo mikali wa Mabudha, Wirathu, amesema hapati usingizi akitakfakari namna ya kukabiliana na Waislamu. Wirathu ambaye ameanzisha 'Harakati ya 969' yenye Mabudha wenye misimamo mikali  wanaoendesha kampeni dhidi ya Waislamu walio wachache  katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya mabudha.
Wiki iliyopita Umoja wa Mataifa umetoa tahadhari kuhusu wimbi jipya la wakimbizi wa Myanmar na Bangladesh wanaoelekea katika eneo la Asia Mashariki na yamkini jambo hilo likaibua maafa ya kibinadamu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR limetaka hatua za haraka zichukuliwe  kabla ya kuanza mvua kali za msimu sambamba na kuanza wimbi la  wakimbizi wapya kutoka Ghuba ya Bengal.
Mwaka huu kumeshuhudiwa wimbi jipya la wakimbizi Waislamu wa kabila la Rohingya wa Myanmar ambao wamekuwa wakikimbia dhulma na ukandamizaji katika nchi hiyo inayotawaliwa na Mabudha..
Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa na makumi ya maelfu ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Mabudha hao wamekuwa wakiungwa mkono na vyombo vya dola. Umoja wa Mataifa pia umetangaza kuwa Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao wanaunda asilimia 5 ya watu milioni 60 nchini Myanmar ni moja kati ya jamii zinazodhulumiwa zaidi duniani.../mh

3359969

captcha