IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Hija ni dhihirisho la adhama, umoja wa Umma wa Kiislamu

6:28 - August 23, 2015
Habari ID: 3350077
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ibada ya Hija ni dhamana ya kuendelea kuwepo Uislamu na dhihirisho la umoja na adhama ya Umma wa Kiislamu.

Ayatullahil Udhma Ali Khamenei ameyasema hayo Jumamosi mjini Tehran katika mkutano na wafanyakazi wa Hija na safari za kuelekea kwenye maeneo matakatifu na kusisitiza umuhimu wa kutiliwa maanani masuala ya kijamii na ya mtu binafsi ya ibada kubwa ya Hija. Amesema kuhamisha uzoefu na tajiriba ya umoja wa taifa la Iran katika mkusanyiko mkubwa wa ibada ya Hija kutapelekea kupatikana mshikamano, umoja na nguvu zaidi kwa Umma wa Kiislamu.
Akizungumzia upande wa kijamii wa ibada ya Hija, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mahudhurio ya mataifa yote yanayotofautiana kimbari, kimadhehebu, kiutamaduni na katika dhahiri yao katika miji ya Makka na Madina na akasema: Hija ni fursa halisi ya umoja na mshikamano wa Kiislamu. Ayatullah Khamenei amekosoa watu wanaotumia mbinu mbalimbali kudhoofisha hakika na umuhimu wa Umma wa Kiislamu ikiwemo mbinu ya kukuza na kutilia chumvi maana ya utaifa na akasema: Hija ni mfano wenye maana wa kuundwa Umma wa Kiislamu na fursa kubwa sana ya kudhihirisha umoja, mshikamano na mfungamano wa Waislamu kote duniani.
Ameashiria uzoefu wa Iran katika kumtambua adui, kutomtegemea na kutofanya makosa katika kuchagua rafiki na akasema: Wananchi wa Iran wameelewa kwamba, ubeberu wa kimataifa na Uzayuni ndio maadui halisi wa Umma wa Kiislamu na kwa sababu hiyo katika mikusanyiko na mijumuiko yote mikubwa ya kitaifa na Kiislamu wamekuwa wakitoa nara dhidi ya Marekani na Uzayuni.
Ayatullah Khamenei ameashiria tajiriba iliyofeli ya kuchukua madaraka baadhi ya makundi ya Kiislamu katika baadhi ya nchi na akasema: Tofauti na taifa la Iran, makundi hayo yalifanya makosa katika kuainisha nafasi ya rafiki na adui na yakapata pigo kutokana na makosa hayo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mapigano ya ndani yanayoshuhudiwa katika baadhi ya nchi kwa visingizio vya kimadhehebu, kisiasa na hata kichama ni matokeo ya kutothamini neema ya umoja. Ameongeza kuwa, watu wasiotambua thamani ya umoja na mshikamano hukumbwa na hitilafu na mapigano.

3349856

captcha