IQNA

Nchi za Ulaya zaunga mkono dola la Palestina

23:09 - November 19, 2014
Habari ID: 1475315
Bunge la Uhispania na Rais wa Slevonia wameunga mkono suala la kutambuliwa rasmi dola la Palestina. Hatua hii inakuja katika wimbi la uungaji mkono wa dola la Palestina.

Wabunge wa Uhispania Jumanne ya jana walipiga kura na kutambua rasmi nchi ya Palestina na kuitaka serikali ya nchi hiyo iitambue rasmi. Awali Waziri Mkuu wa Uhispania Jose Manuel Garcia-Margallo alitangaza kuwa, hatua zinapaswa kuchukuliwa kwa haraka kwa ajili ya kuundwa nchi huru ya Palestina ili kumaliza machafuko katika eneo la Mashariki ya Kati.

Rais wa Slevonia pia amezungumzia jitihada zinazofanywa na nchi yake kwa ajili ya kuitambua nchi ya Palestina. Borut Pahor alisema Jumanne kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kufuatilia kwa haraka mwenendo wa kutambuliwa nchi ya Palestina.

Kufuatia kushindwa mtawalia mazungumzo eti ya upatanishi kati ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel, nchi za Ulaya kutokana na mashinikizo ya ndani na nje na pengine kwa lengo la kuwashinikiza maafisa wa Marekani na Israel, zimeanza mikakati ya kuunga mkono suala la kutambuliwa rasmi nchi la dola la Palestina. Serikali ya Sweden mwezi uliopita ilikuwa nchi ya kwanza mwanachama wa Umoja wa Ulaya kutambua rasmi nchi ya Palestina, suala lililokabiliwa na radiamali kali ya utawala wa Kizayuni. Mabunge ya Ufaransa na Uingereza pia yamependeleza mipango kama hiyo ya kutambuliwa rasmi dola la Palestina. Nchi za Hungary, Poland, Bulgaria, Romania, Malta na Cyprus pia ziliitambua rasmi nchi ya Palestina kabla ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Duru za Marekani zinaeleza kuwa, baadhi ya mabunge ya Ulaya yameitishia Marekani kwamba iwapo haitachukua hatua madhubuti za kuhuisha mazungumzo ya upatanishi, zitaitambua rasmi kwa pamoja nchi ya Palestina. Kwa sasa kadhia hiyo imezusha mjadala mkubwa katika Umoja wa Ulaya (EU). Japokuwa kukosekana sera za pamoja katika EU kumemfanya kila mwanachama wa jumuiya hiyo achukue msimamo wake binafsi juu ya kadhia hiyo, lakini viongozi wa Israel na waitifaki wao wa Magharibi, wanazidi kutiwa wasiwasi na mwenendo huo wa nchi za Ulaya wa kuzidi kuunga mkono dola ya Palestina.

Kwa sababu hiyo, lobi za Kizayuni zinafanya jitihada kubwa ya kuzuia kupigwa kura katika mabunge ya nchi za Ulaya ili kutambuliwa nchi ya Palestina. Hata hivyo weledi wa mambo hawana matumaini na mwenendo huo mpya ulioanzishwa na nchi za Ulaya wa kuitambua nchi ya Palestina, na wanasema kwamba mpango huo ni kwa ajili ya mikakati ya kuuimarisha zaidi utawala wa Kizayuni na kuwashinikiza Wapalestina ili waendelee na mazungumzo eti ya upatanishi.

Kwa msingi huo, hatua hiyo ya nchi za Ulaya ya kuitambua nchi ya Palestina ambayo haitabadili siasa za serikali ya Israel, inaweza kuwa kwa ajili ya kuvutia fikra za waliowengi duniani. Huwenda ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Umoja wa Ulaya umeisisitizia Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwamba, hautaitambua rasmi nchi ya Palestina iwapo mazungumzo na Israel yataendelea kusimama.../mh

1474919

captcha