IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Uswidi: Msikiti waharibiwa vibaya katika hujuma ya uchomaji moto

21:26 - September 26, 2023
Habari ID: 3477654
STOCKHOLM (IQNA) - Msikiti mmoja kusini mashariki mwa Uswidi umeharibiwa vibaya kufuatia shambulio la uchomaji moto.

Akizungumza na shirika la utangazaji la umma SR, mkurugenzi wa mawasiliano wa Msikiti Mkuu wa Eskilstuna Anas Deneche amethibitisha moto huo ulisababishwa na hujuma ya uchomaji moto.

Msikiti huo uko katika sehemu ya Arby ya mji wa Eskilstuna.

Rekodi za polisi zinaonyesha msikiti huo umekabiliwa na vitisho kabla ya shambulio hilo la uchomaji moto.

Polisi wanasema kuwa msikiti huo hauwezi kutumika kutokana na uharibifu huo na kwamba uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hilo.

Hakuna aliyejeruhiwa wakati wa moto huo ambao ulizimwa na wazima moto waliotumwa kutoka vituo vinne.

Deneche anasema kuwa hawakusudii kukata tamaa bali msikiti huo kwa namna fulani utajengwa upya. Hadi wakati huo, anawataka wanachama kuwa na subira.

"Tunapata kufanya kile ambacho sisi Waislamu tunasema 'sabar', ambayo ni uvumilivu," alisema.

Moto huo umekuja huku kukiwa na msururu wa mashambulizi dhidi ya Uislamu na Qur'ani Tukufu nchini Uswidi katika miezi michache iliyopita huku watu wenye itikadi kali wakitumia vibaya sheria za uhuru wa kujieleza za nchi hiyo ya Skandinavia kuendeleza chuki dhidi ya Waislamu.

Kutokuwa na uvumilivu kwa Waislamu kunaongezeka katika nchi za Ulaya zinazodai kuwa watetezi wa demokrasia na uhuru wa kuabudu.

Kishikizo: sweden msikiti waislamu
captcha