IQNA

Al-Masjid an-Nabawi

Waislamu milioni nne watembelea Msikiti wa Mtume SAW mjini Madina katika kipindi cha wiki moja

16:19 - July 05, 2023
Habari ID: 3477242
MADINA (IQNA) - Zaidi ya mahujaji milioni nne wametembelea Msikiti wa Mtume SAW ambao ni maarufu kama Al-Masjid an-Nabawi huko Madina katika wiki moja, mamlaka ya Saudi inasema.

Kwa mujibu wa Urais Mkuu wa Msikiti wa Mtume SAW, watu 4,252,000 walitembelea na kuswali katika Msikiti wa Mtume SAW katika mji mtakatifu wa Madina kati ya Juni 25 na Julai 02, 2023.

Hiki kilikuwa ni kipindi cha tarehe 7 hadi 14 Dhu Al Hijjah katika mwaka wa 1444 Hijria Qamaria ambapo Mahujaji wengi walisafiri hadi Madina baada ya kumaliza ibada zao tukufu huko Makka.

Ofisi ya Urais Mkuu wa Msikiti wa Mtume SAW ilisema inaratibu na mamlaka mbalimbali zinazosimamia ulinzi, afya, huduma, na kujitolea ili kuhakikisha kuwa wageni na waumini wanapata uzoefu mzuri na wa kustarehesha wanapotekeleza majukumu yao ya kidini.

Miongoni mwa huduma zilizotolewa na Urais wa Al-Masjid an-Nabawi ni ugawaji wa chupa 203,294 za maji ya Zamzam, ambayo kwa mujibu wa itikadi ya Kiislamu ni maji matakatifu  na yaliyobarikiwa.

Masjid An Nabawi ni msikiti wa pili mtakatifu zaidi katika Uislamu, baada ya Masjid al-Haram huko Makka, na huvutia mamilioni ya wageni wacha Mungu kila mwaka. Msikiti huo ulianzishwa na Mtume Muhammad (SAW) mwenyewe alipohamia Madina mwaka 622 Miladia. Ni msikiti wa pili kwa ukubwa duniani, na umefanyiwa upanuzi kadhaa kwa karne nyingi ili kukidhi ongezeko la idadi ya waabudu.

Msikiti huo pia ndipo alipozikwa Mtume Muhammad (SAW) chini ya kuba la kijani kibichi lenye minara ya marumaru nyeupe.

3484213

Kishikizo: al masjid an nabawi
captcha