IQNA

Ajali ya Winchi

Shirika la Binladin latozwa faini ya dola milioni 5.32 kwa ajali ya winchi katika Msikiti wa Makka

17:27 - February 15, 2023
Habari ID: 3476565
TEHRAN (IQNA) - Mahakama ya Saudia imetoa uamuzi wa ajali ya winchi iliyotokea mwaka 2015 katika Msikiti Mkuu wa Makka ambayo iliua takriban watu 109.

Uamuzi wa mahakama ya rufaa ambao unakuja baada ya miaka saba umelitoza Shirika la Binladin la Saudia faini ya riyal milioni 20 (dola milioni 5.32) baada ya kulipata na hatia ya uzembe na ukiukaji wa usalama.

Ikumbukwe kuwa mnamo Septemba 11 mwaka 2015, winchi kubwa ya ujenzi ilianguka wakati kukiwa na upepo mkali katika Msikiti Mtakatifu wa Makka na kuwaua waumini 109 na kuwajeruhi wengine 200 kabla ya kuanza Ibada ya Hija.

Winchi hiyo ilikuwa mojawapo ya nyingi ambazo kampuni hiyo ya ujenzi ilikuwa imejenga kama sehemu ya mpango wa upanuzi wa masikiti huo uliogharimu  mabilioni ya dola ili kuweza kuhudumia idadi inayoongezeka ya Mahujaji.

Mahakama ya Rufaa ya Jinai mjini Makka aidha imeamua kwamba kampuni hiyo haikuhitajika kulipa fidia kwa jamaa za waliouawa kwenye ajali hiyo.

Watu saba walipatikana na hatia, huku watatu wakihukumiwa kifungo cha miezi sita jela na kutozwa faini ya hadi riyal 30,000 huku wanne wakipokea vifungo vya miezi mitatu jela na kutozwa faini ya riyal 15,000.

Mnamo mwaka wa 2017, mahakama ya rufaa iliamuru kusikilizwa kwa kesi mpya iliyohusisha takriban watu kumi na wawili wanaoshutumiwa kwa uzembe, baada ya mahakama ya chini kuliondoa hatiani shirika hilo la Binladin.

Shirika hilo linamilikiwa na familia ya Bin Laden, ambayo ina uhusiano wa karibu na ukoo wa Aal Saud unaotawala Saudi Arabia. Binladin linatambulika kama shirika la pili kwa ukubwa la ujenzi duniani baada ya Shirika la Ujenzi la Vinci la Ufaransa. Binladin lina makao yake mjini Jeddah na ilianzishwa mwaka 1931 na Sheikh Mohammed bin Laden, baba yake Osama bin Ladin kinara aliyeuawa wa kundi la kigaidi la al Qaeda.

Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Ujenzi la Binladin, shirika hilo limehusika katika ujenzi wa miradi muhimu Saudia kama vile jingo la al-Faisalia mjini Riyadh, Kituo cha Kifedha cha Mfalme Abdullah, vyuo vikuu kadhaa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Abdul Aziz mjini Jeddah.

3482487

captcha