IQNA

Jinai za Israel

Walowezi wa Kizayuni wavamia Msikiti wa Al-Aqsa wakati wa hujuma dhidi ya Gaza

17:17 - August 07, 2022
Habari ID: 3475592
TEHRAN (IQNA) – Idadi kubwa ya walowezi wa Kizayuni wenye itikadi kali waliuvamia na kuuvunjia heshima Msikiti wa Al-Aqsa mjini Quds (Jerusalem) mapema Jumapili wakati utawala dhalimu wa Israel uikuwa ukiwashaambulia na kuwaua Wapalestina kwa mabomu huko Gaza kwa siku ya tatu mfululizo.

Wakilindwa na askari katili wa Israel waliokuwa wamejizatiti kwa silaha nzito nzito, walowezi wa Kizayuni walianza uvamizi huo mapema Jumapili asubuhi kwa saa za huko na kuendelea kwa saa tatu, katika siku ambayo kulikuwa kunaadhimishwa sikukuu ya Kiyahudi ya Tisha B'av.

Uvamizi hui umeandaliwa na vikundi vya Kizayuni vyenye siasa kali za mrengo wa kulia vinavyotaka kuharibiwa kwa Msikiti wa Al-Aqsa, mojawapo ya maeneo takatifu zaidi katika Uislamu.

Walowezi wa Kizayuni waliinua benera za Israel huku wakitekeleza ibada za Kiyahudi ndani ya uwanja wa Msikiti wa Al Aqsa.

Kama sehemu ya maelewano ya miongo kadhaa kati ya Jordan - mlinzi wa maeneo ya Kiislamu na Kikristo huko Jerusalem - na Israel, wasio Waislamu hawaruhusiwi kufanya ibada zozote za kidini ndani ya mipaka ya Msikiti wa Al-Aqsa, na alama za Israel haziruhusiwi kuonyeshwa katika msikiti huo.

Wasio Waislamu wanaweza kuzuru msikiti huo chini ya usimamizi wa Idara ya Wakfu wa  pamoja wa Jordan na Palestina ambayo inasimamia masuala ya msikiti huo.

Mbunge wa mrengo mkali wa kulia Itamar Ben-Gvir aliongoza moja ya makundi yaliyovamia msikiti huo, katika kile ambacho Wapalestina wanaona kuwa ni uchochezi wa hisia zao na kudhalilisha utakatifu wa msikiti huo.

Ben-Gvir, ambaye anaishi katika makazi haramu katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ni mkuu wa chama kidogo cha Jewish Power na anahusishwa na itikadi kali ya Khanist iliyo dhidi ya Wapalestina.

Kulingana na vyombo vya habari vya Palestina, takriban Wazayuni 1,000 walivamia msikiti huo Jumapili

Vikundi vidogo vya waumini wa Kiislamu waliokuwa ndani ya msikiti huo wakati wa uvamizi huo walihujumiwa na kukandamizwa na wanajeshi wa Israel.

Nje ya msikiti huo, ulioko katika Jiji la Kale la Quds, mapigano yalitokea kati ya Waisraeli wenye msimamo mkali na wakaazi wa Palestina.

Uvamizi wa Wazayuni  dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa siku ya Jumapili uliruhusiwa na mamlaka ya Israel licha ya wasiwasi kwamba hatua hiyo inaweza kuzua ghasia zaidi wakati wa kampeni ya kinyama ya kijeshi ya Israel inayoendelea huko Gaza.

Zaidi ya Wapalestina 31 wakiwemo watoto sita wameuawa katika mashambulizi hayo yaliyoanza siku ya Ijumaa. Takriban 253 walijeruhiwa, zaidi ya nusu yao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya ya Palestina.

Siku ya Jumamosi, maandamano kadhaa yaliandaliwa na Wapalestina kulaani uvamizi wa Israel huko Haifa, Jaffa, Ramallah, Al Khalil na Quds, miongoni mwa miji mingine ya Wapalestina.

3480008

captcha