Kila mwaka na katika Ijumaa ya kwanza ya mwezi wa Muharram, kwa mnasaba wa kukumbuka alivyouawa shahidi kikatili Ali Asghar, mtoto mchanga wa miezi sita wa Imam Hussein (AS), Imam wa tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani, hufanyika kongamano na mjumuiko maalumu unaoshirikisha akina mama na watoto wao wachanga wanaonyonya.
Mijumuiko hiyo ijulikanayo kama 'Vichanga Vinyonyavyo vya Imam Hussein (AS)' , imefanyika kote nchini Iran na katika nchi zingine duniani ikiwemo India, Pakistan, Bahrain, Iraq, Saudi Arabia, Uturuki, Afghanistan, Nigeria n.k, ambapo akina mama wamewawekea nadhiri watoto wao kwa ajili ya mapambano ya Imam wa Zama, Imam Mahdi (AS), ambaye ni Imamu wa 12 na wa mwisho wa Waislamu wa Kishia.
Hapa mjini Tehran, shughuli hiyo imefanyika katika Uwanja Mkuu wa Sala wa Imam Khomeini (MA), ambapo akina mama waliokuwa wamebeba watoto wao wachanga waliomboleza masaibu na mateso yaliyompata Imam Hussein (AS).
Imam Hussein (AS) ambaye kwa kujitolea kwake mhanga kusio na kifani aliuawa shahidi Siku ya Ashura, yaani tarehe 10 Muharram katika ardhi ya Karbala, amewaachia walimwengu wote somo kubwa la maana halisi ya kukomboka na kuwa na izza na heshima.
Katika siku hiyo ya Ashura katika jangwa la Karbala Imam Hussein (AS) alisisitiza kuwa: "kusudio langu ni kuufedhehesha utawala ulio dhidi ya Uislamu, kuamrisha mema na kukataza maovu na kusimama dhidi ya dhulma na uonevu".
Mafunzo yaliyomo kwenye harakati ya Imam Hussein (AS) yamevuka mipaka ya historia na jiografia na kujumisha wanadamu wote ulimwenguni.
3479985