IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika

Mwanamke Muirani ametoa pigo kubwa kwa madai ya uongo wa Wamagharibi

7:22 - July 28, 2022
Habari ID: 3475550
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Mwanamke mwenye hadhi na kipaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa pigo kubwa na muhimu zaidi kwa madai na uongo ya ustaarabu wa Magharibi, na suala hilo limewakasirisha mno Wamagharibi.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo Jumatano mjini Tehran katika hadhara ya maimamu wa Swala za Ijumaa waliokwenda kukutana naye kutoka maeneo mbalimbali ya Iran. Ameashirii maudhui ya mwanamke na vazi la hijabu na kuongeza kuwa: Masuala haya daima yamekuwa yakiibuliwa tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na sasa, majaribio yaleyale yaliyofeli yanarudiwa kwa kisingizio cha vazi la hijabu.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Miaka michache iliyopita niliulizwa katika kikao kwamba, una hoja gani ya kujitetea mbele ya nchi za Magharibi kuhusiana na suala la wanawake, nikasema: "Sihitaji kujitetea, bali ninashambulia; Wale ambao wamewageuza wanawake kuwa bidhaa ndio wanaolazimika kujitetea na kutoa majibu."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza swali: "Kwa nini vyombo rasmi vya habari na vya serikali vya Marekani na Uingereza na mamluki wao vimefanya mashambulizi tena kuhusu suala la wanawake kwa kisingizio cha vazi la hijabu? Na je, watu wa Magharibi ni watetezi kweli wa haki za wanawake wa Iran?", na kusema: Wamagharibi hawa wanaodai kutetea haki za wanawake wa Iran, ndio wale wale ambao lau wangeweza kulifungia maji taifa la Iran, wangeyafunga, sawa kabisa na ambavyo wamepiga marufuku dawa za watoto wenye ugonjwa wa kipepeo kuingia Iran na hawaruhusu dawa ugonjwa huo kuwafikia watoto hao. Amehoji akisema: Je, ni kweli kwamba watu wa Magharibi wanawaonea huruma wanawake wa Iran?

Ayatullah Khamenei amesema: Wamagharibi wamekuwa wakisema kwa miaka mingi kwamba wanawake hawawezi kuendelea na kufikia viwango vya juu vya elimu na sayansi, siasa na jamii hadi watakapokombolewa kutoka kwenye mipaka ya maadili na sheria za dini; lakini tumeona kuwa katika miaka arubaini iliyopita, wanawake wa Kiirani wameweza kujitokeza katika nyuga mbalimbali za kisayansi, kijamii, kimichezo, kisiasa, kiuongozi, kiuchumi na kiutamaduni wakiwa na vazi la hijabu na chador ya Kiislamu na kupata mafanikio na fahari kubwa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kazi kubwa iliyofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kubatilisha fikra kuu ya utambulisho wa ustaarabu wa kimagharibi, yaani "kutenganisha dini na siasa", na kusema: Jamhuri ya Kiislamu si tu kwamba imeweza kujilinda kwa kutumia kaulimbiu ya dini, bali kwa maendeleo ya sasa ya Iran, ilitoa changamoto kwa juhudi za muda mrefu za Wamagharibi za kutaka kuonesha kwamba, dini na siasa ni vitu viwili visivyoendana. Kwa hiyo, mafia wa madola ya Magharibi, wakiongozwa na Wazayuni na mabepari wao, na vilevile Marekani, wamekasirishwa na ukweli huu adhimu, na daima wanapanga njama za kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu.

/4073766

captcha