IQNA

Ukombozi wa Palestina

Haniya: Ukombozi wa Msikiti wa Al Aqsa unakaribia

17:22 - June 26, 2022
Habari ID: 3475427
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisisitiza kuhusu utambulisho wa Kiislamu wa Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds (Jerusalem) na kuongeza kuwa, wanaosaliti Palestina kwa kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel wafahamu kuwa ukombozi wa Msikiti wa Al Aqsa unakaribia.

Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameyasema hayo kusini mwa Lebanon leo alipohutubu katika sherehe mjini Saida. Amesema Msikiti wa Al Aqsa si eneo la Mayahudi na Wazayuni na ndogo yao ya kutwaa eneo hilo takatifi la Kiislamu itaambulia patupu.

Kwingineko, Haniya amesema mapambano na muqawama ungali unaongeza nguvu zake hadi ufike wakati wa kukombolewa Palestina iliyoanzia Mto Jordan hadi Bahari ya Mediterania.

Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, aliyekuwa akihutubia kongamano la mirengo ya kitaifa na Kiislamu jana katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut ameeleza katika hotuba yake kwamba, Saiful-Quds (Upanga wa Quds) ni nukta yenye umuhimu wa kipekee katika mchakato na vuguvugu la mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Haniya amesisitiza kwa kusema: "sisi tunawajua vizuri maadui, tumepigana vita nao magerezani na kwenye mitaa ya Palestina na hii leo muqawama wa Palestina umefikia hatua ya kuufanya utawala wa Kizayuni usithubutu kuanzisha hujuma".

Kiongozi huyo wa Hamas ametahadharisha pia kuhusu hatari ya utawala wa Kizayuni kujumuishwa kwenye miungano ya kijeshi ya ukanda huu na akaongezea kwa kusema: "inapasa medani zote za mapambano na kambi zote za muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni ziungane na kuwa kitu kimoja".

Ismail Haniya amezungumzia pia ukiukaji wa mipaka ya bahari ya Lebanon unaofanywa na utawala wa Kizayuni na akasisitiza kwa kusema: "sisi tunaiunga mkono Lebanon katika kunufaika na haki yake katika Bahari ya Mediterania".

Kuhusu matukio yanayoendelea kujiri katika eneo, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesema: "kinachoendelea kujiri katika eneo ni hatari kubwa zaidi kuliko kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni".

4066784

captcha