IQNA

Rais Raisi wa Iran katika mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki

Iran na Uturuki zijiandae kuimarisha uhusiano wa pande zote

19:53 - November 15, 2021
Habari ID: 3474561
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo hapa Tehran na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki na kusisitiza kuwa: Iran na Uturuki zinapasa kujiandaa kuimarisha uhusiano wa sasa kuelekea kwenye ushirikiano wa pande zote.

Katika mazungumzo yake ya leo na Mevlut Cavusoglu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Rais Sayyid Ebrahim Raisi ameashiria namna kustawisha uhusiano kati ya nchi mbili hususan katika uga wa kibiashara na kiuchumi kutayanufaisha mataifa mawili na kueleza kuwa: Iran na Uturuki zinapasa kujiandaa kuimarisha uhusiano wa sasa ili kukuza ushirikiano wa pande zote kwa kukamilisha ramani ya njia ya ushirikiano wa nchi mbili.  

Rais wa Iran ameongeza kuwa, ushirikiano wa kikanda wa nchi mbili unapasa kustawi zaidi na kuwa ushirikiano wa kimataifa na kwamba kwa kuzingatia nafasi muhimu ya nchi hizi mbili, aina hii ya maingiliano inaweza kuwa na ufanisi katika masuala ya kimataifa.

Rais Ebrahim Raisi ameashiria mtazamo wa Iran unaoamini kwamba nchi za eneo hili zina uwezo wa kutatua masuala na matatizo yao bila ya uingiliaji wa nchi ajinabi na kueleza kuwa: Matokeo ya uwepo wa nchi za kigeni katika kanda hii ni  ukosefu wa amani na kuibua mivutano kati ya nchi na mataifa ya eneo hilo kama ambavyo uwepo wa miaka 20 wa Marekani huko Afghanistan hakuwa na matokeo mengine isipokuwa kusabababisha mauaji, umwagaji damu na maafa. Amesema, ni wazi kwamba matatizo ya Afghanistan yanaweza kupatiwa ufumbuzi na wananchi wa nchi hiyo na msaada wa nchi jirani.  

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Rais wa Iran amebainisha kuwa, kupambana na ugaidi na uhalifu wa kupaga kunaweza kuwa ajenda za ushirikiano kati ya Tehran na Ankara na kwamba Iran iko tayari kupandisha kiwango cha ushirikiano katika uwanja huo.

Mevlut Cavosoglu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki pia amesisitiza kuwa nchi yake inataka kuzidisha kasi ya kuimarishaji uhusiano wake na Iran na kwamba Ankara. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameongeza kuwa Ankara inataka kuimarisha na kuboresha ushirikiano wa pamoja na Iran kwa kuzidisha hali ya utulivu na uhusiano wa kibiashara eneo la Kaukasia Kusini.

4013505

Kishikizo: iran uturuki raisi
captcha