IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Watu wa Iran wataonyesha fahari na heshima ya taifa kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi

2:12 - June 17, 2021
Habari ID: 3474012
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa wanachi wa Iran wataonyesha fahari na heshima ya taifa kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa rais utakaofanyika Ijumaa ijayo.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika hotuba yake kwa taifa na kuongeza kuwa, chini ya masaa 48 yajayo kutashuhudiwa tukio jingine muhimu sana hapa nchini ambalo ni uchaguzi wa Rais na Mabaraza ya Miji na Vijiji. 

Amesema kuwa, mustakbali wa nchi katika masuala yote ya kiuchumi, utamaduni, usalama, afya na kadhalika unategemea uamuzi wa wananchi siku ya Ijumaa ijayo, Inshaallah, na kwamba mahudhurio makubwa ya wananchi katika zoezi hilo na kura zao vitakuwa na nafasi muhimu katika mustakbali wa taifa kwenye masuala mbalimbali. 

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kushiriki wananchi kwenye maamuzi ya kitaifa kwenye mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni msingi na nguzo muhimu ya kifikra na wala si suala la kisiasa tu. Amesema japokuwa kushiriki huko kwa wananchi kuna faida nyingi za kisiasa lakini muhimu zaidi ni falsafa ya kushirikishwa wananchi katika masuala ya utawala kwenye mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, kwa maana kwamba, katika Jamhuri ya Kiislamu kuna "Jamhuri" yaani watu na "Uislamu"; na iwapo wananchi hawatashirikishwa basi Jamhuri ya Kiislamu haitakamilika. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, lengo la adui ni kutaka uchaguzi ujao usifanyike vizuri na inavyotakikana na kuona wananchi wanajitenga na utawala. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, wananchi wengi wameonesha kuwa, daima wanakwenda na kutenda kinyume na matakwa ya adui katika masuala mengi kama katika chaguzi na maandamano yanayofanyika hapa nchini. Amesema hali itakuwa hivyo hivyo pia mara hii kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu na wananchi watashiriki kwa wingi katika zoezi la kupiga kura na kuinua juu hadhi na heshima ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  

3978035

captcha