IQNA

Sayyid Nasrallah: Hatimaye sote tutaswali katika Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa

13:43 - June 09, 2021
Habari ID: 3473993
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema hakuna chembe ya shaka kuwa Waislamu karibuni hivi wataibuka washindi mkabala wa Wazayuni na waitifaki wao, na hatimaye watatekeleza ibada ya Swala katika Msikiti mtukufu wa al-Aqsa, huko Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu.

Sayyid Hassan Nasrallah alisema hayo jana Jumanne katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni na kusisitiza kuwa, "ningali na matumaini kuwa hatimaye sote tutaswali katika Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa."

Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wakipewa ulinzi na wanajeshi wa utawala pandikizi wa Israel wamekuwa wakiuhujumu Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu. 

Sayyid Nasrallah ameashiria kuhusu maadhimisho ya mwaka wa 54 wa kumbukumbu ya Siku ya Naksa huko Palestina, inayokumbusha vita kati ya Israel na nchi za Kiarabu za Misri, Syria na Jordan na kubainisha kuwa, vita hivyo vilifungua mlango wa kukaliwa kwa mabavu maeneo mengi ya Asia Magharibi, kama Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan uliko mji mtukufu wa Quds, mashamba ya kilimo ya Shebaa ya Lebanon na Miinuko ya Golan ya Syria.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, tangu vita hivyo vya mwaka 1967 vijiri, Wapalestina wamesimama kidete kwa miongo mingi na kujitolea muhanga katika mapambano ya kuuhami na kulinda historia na muundo wa mji mtukufu wa Quds na Msikiti wa al-Aqsa. 

Kuhusu kumbukizi ya mwaka wa 32 wa kufariki dunia mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, Imam Khomeini (MA), Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa, Imam Ruhullah aliupuliza pumzi ya uhai Umma wa Kiislamu, na kuhuisha moyo wa muqawama na mapambano dhidi ya dhulma.

3474922

Kishikizo: nasrallah aqsa hizbullah
captcha