IQNA

Tawala za Israel na Saudia kutangaza uhusiano rasmi baina yao

16:53 - December 09, 2018
Habari ID: 3471765
TEHRAN (IQNA)- Uhusiano rasmi baina ya Utawala wa Kizayuni wa Israel na Utawala wa Kifalme Saudi Arabia unatazamiwa kutangazwa rasmi katika kipindi cha miezi michache ijayo.

Hayo yamedokezwa na Kanali mashuhuri ya televisheni ya Hadashot ya utawala haramu wa Israel ambayo imetangaza kuwa, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu anataka kuhakikisha kuwa jambo hilo linafanikiwa kabla ya uchaguzi mkuu wa utawala huo uliopangwa kufanyika Novemba 2019.

Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la mikutano ya siri na ya dhahiri baina ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia katika fremu ya kuandaa uhusiano wa kawaida baina ya pande mbili.

Mwezi Aprili, Gazeti la al Manar la Palestina lilichapisha ripoti iliyosema kuwa, mfalme wa Saudi Arabia ndiye muhandisi wa uhusiano wa Wasaudia na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuandika kuwa: Tangu mwanzoni mwa mwaka 1990, mfalme wa hivi sasa wa Saudia ana uhusiano wa karibu na Israel.

Uhusiano wa Mfalme Salman na Rabin

Gazeti hilo la Palestina limezinukuu duru za kuaminika zikifichua kuwa: Mawasiliano ya siri na ya kificho baina ya Salman bin Abdulaziz Aal Saud, mfalme wa hivi sasa wa Saudi Arabia na Israel yamekuwepo tangu Salman alipokuwa amir wa Riyadh. Tangu wakati huo alikuwa na mawasiliano ya karibu na watu kama Is'haq Rabin, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Ripoti ya gazeti hilo imesisitiza kuwa, Salman alimuunganisha mwanawe Muhammad bin Salman kwenye mawasiliano hayo maalumu na Israel tangu miaka kadhaa nyuma.

Kesi ya Khashoggi

Mapema mwezi huu wa Disemba,  gazeti la New York Times la Marekani lilifichua kuwa, shirika moja la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilitoa msaada mkubwa wa kijasusi kwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia ili kufanikisha mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala huo wa kiimla.

Saudi Arabia ilishirikiana na Israel katika kueneza migogoro na kuibua makundi ya kigaidi ambayo yamevuruga amani Syria na Iraq. Aidha tawala za Riyadh na Tel Aviv zinashirikiana katika hujuma dhidi ya Yemen tokea Machi 2015 ambapo watu zaidi ya 13,000, wengi wakiwa ni watoto na wanawake wameuawa na mamilioni ya wengine kuachwa bila makao.

Quds Tukufu

Juhudi za waziwazi za Saudia za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni zinafanyika katika hali ambayo kwenye miaka ya hivi karibuni, mbali na Israel kuwakandamiza vibaya Wapalestina na kuendelea kuteka ardhi zao na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, inaendelea pia kuzikalia kwa mabavu ardhi nyingine za Kiarabu-Kiislamu hasa kibla cha kwanza cha Waislamu, yaani Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds.

3467410

captcha