IQNA

Wenye Chuki na Uislamu watangaza "Siku ya Kumwadhibu Muislamu" Uingereza

9:08 - March 12, 2018
Habari ID: 3471426
TEHRAN (IQNA)- Wasiwasi umetanda katika jamii ya Waislamu nchini Uingereza baada ya kundi lenye chuki dhidi ya Uislamu kusambaza barua za kuhimiza kuhujumiwa Waislamu na misikiti nchini humo.

Taarifa zinasema wakaazi wa mji wa London na maeneo ya West Midlands na Yorkshire wamesema wamepokea barua hizo, zinazowataka kufanya hujuma dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada mnamo Aprili 3, siku ambayo wameitaja kuwa  'Siku ya Kumwadhibu Muislamu'.

Sehemu moja ya barua hiyo imetangaza zawadi ya pointi 10 kwa kumshambuliwa kwa matusi Muislamu, pointi 50 kwa yule atayemwagia tindikali Muislamu, pointi elfu moja kwa atakayeshambulia msikiti, na pointi 2,500 kwa yule atakayeishambulia kwa silaha za nyuklia kibla cha Waislamu, Al Kaaba, katika mji mtakatifu wa Makka.

Miqdaad Versi, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Uingereza amelaani vikali kusambazwa barua hizo zinazoashiria kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, lakini pia amebainisha kuwa kitendo hicho kimewaweka Waislamu wa nchini Uingereza katika hali ngumu. Aidha ametoa wito kwa polisi kuwakamata wanaoeneza barua hiyo ya chuki na kuwafikisha kizimbani.

Kuna Waislamu karibu milioni tatu Uingereza na hivyo kuufanya Uislamu kuwa dini ya pili kwa ukubwa nchini humo.

Tell MAMA, taasisi inayochunguza vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu na kusema hali ya taharuki imeenea katika jamii ya Waislamu nchini Uingereza.

“Barua hii imeibua hofu kubwa katika jamii,” amesema Iman Atta, mkurugenzi wa Tell MAMA.

Ameongeza kuwa, “Waislamu wanauliza iwapo itakuwa salama watoto kucheza nje. Tumewaambia watulie na wajulishe polisi punde wakipokea barua hizo.”

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Waislamu barani Ulaya hususan Uingereza, katika miaka ya hivi karibuni wameanzisha kampeni za kuwafahamisha wasiokuwa Waislamu mafundisho ya Uislamu ili kuondoa fikra potofu miongoni mwao kuhusiana na dini hii.

Mwezi uliopita wa Februari, Jeremy Corbyn kiongozi wa chama cha Leba cha nchini Uingereza alisema kuwa, chuki dhidi ya Uislamu ni tatizo kwa jamii ya nchi hiyo ya bara Ulaya na kwamba, dini ya Uislamu ni nembo ya amani na kujitolea.

Jeremy Corbyn  alisema hayo katika msikiti wa Finsbury  kaskazini mwa London katika kampeni ya nchi nzima nchini Uingereza iliyoendeshwa na Waislamu na ambayo inajulikana kwa jina la "Tembelea Msikiti Wangu" na kubainisha kwamba, uhalifu unaofanywa kwa sababu ya chuki dhidi ya Uislamu unatia aibu.

3698768

captcha